UFUNGUZI WA MSIMU WA KAHAWA 2020/2021
20
Aug

UFUNGUZI WA MSIMU WA KAHAWA 2020/2021

Utangulizi


Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania anawatangazia ufunguzi wa msimu mpya wa ununuzi wa kahawa kwa mwaka 2020/2021. Tangazo hili linatolewa kwa mujibu wa kanuni ya 23 (1) ya Kanuni za Kahawa 2013. Pamoja na tangazo hili, Bodi inatoa mwongozo na utaratibu mahsusi kuhusu utaratibu wa masoko ya kahawa kwa mujibu wa kanuni ya 63 ya Kanuni za Kahawa 2013. Tarehe za ufunguzi wa msimu wa kuanza kwa ununuzi wa kahawa katika kanda za uzalishaji kahawa ni kama ifuatavyo;

No. Zone Region Commencement Date
7. Northern Zone Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Morogoro,
Tanga
1st July, 2020
8. Southern
Highlands Zone
Mbeya, Songwe, Katavi 1st June, 2020
9. Kigoma Zone Kigoma 1st May, 2020
10. Mara Zone Mara, Mwanza 1st June, 2020
11. Western Zone Kagera 1st June, 2020
12. Southern Zone Ruvuma, Iringa, Njombe 1st July, 2020

 

Mambo muhimu ya kuzingatia katika msimu huu 2019/2020:

  1. Wanunuzi binafsi na wenye viwanda wanaruhusiwa kununua kahawa kutoka kwa wakulima moja kwa moja kwa kupitia vyama vya Ushirika vya Msingi na vyama vikuu (Union). Kahawa itakayonunuliwa katika soko hili ni ile ambayo imepitia utayarishaji ngazi ya awali (Dry Cherry na Parchment). Wanunuzi wa kahawa watakaotaka kununua kahawa katika soko hili watatakiwa kuwa na leseni za kununua kahawa zinazotolewa na Bodi ya Kahawa kwa mujibu wa sheria ya kahawa na kanuni zake (Parchment Buyers Licence & Dry Cherry Buying Licence). Wanunuzi hawa watapaswa kuingia makubaliano na chama cha ushirika husika yatakayoonyesha kiasi na bei ya kahawa itakayotolewa na mnunuzi wa kahawa.Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya kwa kuzingatia kifungu Na. 26 (2) na Na. 38(5) cha kanuni ya kahawa ya mwaka 2013 watatoa vibali kwa wanunuzi wa kahawa kwenye Halmashauri zao ikiwa ni moja ya masharti ya kupata leseni ya ununuzi kutoka Bodi ya Kahawa.

  2. Katika msimu huu Bodi ya Kahawa Tanzania itaendelea na utaratibu wa kuendesha minada katika kanda za uzalishaji kahawa katika maeneo yafuatayo:
    - Bukoba: Kwa ajili ya Mikoa ya Kagera, Mwanza – Minada itaendeshwa kama kutapatikana kiasi cha kahawa cha        kutosha kuendesha minada.
    - Mbozi: Kwa ajili ya Mikoa ya Songwe, Mbeya, Iringa na Katavi
    - Mbinga: Kwa ajili ya Mikoa ya Ruvuma na Njombe

    Minada ya kanda itaendelea kuwa ni ya kahawa safi na itafanyika kwa mujibu wa kanuni na taratibu za uendeshaji minada zilizopo. Mnada wa kitaifa unaofanyika Moshi utaendelea kufanyika kwa taratibu zilizipo na vyama vya ushirika vitakuwa huru kuchagua soko wanaloliona lina tija kwa kuuza kahawa ya wanachama wao.

  3. Katika msimu huu utaratibu wa soko la moja kwa moja (Direct Export) kwa kahawa aina ya Robusta na Arabika ngumu utakuwa ni kama ulivyoboreshwa msimu uliopita ambapo Vyama vya Ushirika vitatangaza kiasi cha kahawa wanachotarajia kuzalisha kwa madaraja na ubora kupitia tovuti ya Bodi ya Kahawa, Soko la Bidhaa (TMX) na Tume ya Maendeleo ya Ushirika na muda ambao kahawa itakuwa tayari. Wanunuzi wa kahawa kupitia mfumo wa soko la moja kwa moja watawasilisha

    mapendekezo yao ya bei kwa Bodi ya Kahawa yakiainisha yafuatayo;

    i. Kiasi na aina ya kahawa kwa kila daraja.
    ii. Ubora wa kahawa.
    iii. Muda/mwezi ambao wanatarajia kuchukua kahawa husika.
    iv. Bei anayotarajia kulipa kwa kila daraja la kahawa kwa kuzingatia utaratibu wa bei ya soko, muda wa ununuzi na ubora wa kahawa.

    Mapendekezo ya bei yaliyowasilishwa na wanunuzi wa kahawa yatashindanishwa kupitia utaratibu utakaokuwa unasimamiwa na Bodi ya Kahawa na Soko la Bidhaa (TMX) na matokeo yatawasilishwa kwa Vyama vya Ushirika kwa makampuni yaliyotoa bei ya juu ili vyama hivyo viweze kuingia makubaliano ya kuuza kahawa kwa washindi hao kupitia utaratibu wa soko la moja kwa moja au kwa wanunuzi wengine watakaoweza kutoa bei kubwa zaidi ya mshindi. Bei halisi ya kahawa katika makubaliano hayo itafikiwa wakati wa kuchukua kahawa.
  4. Maombi ya leseni zote mpya yatafanyika kwa kutumia mtandao katika mfumo wa ATMIS kwa kufuata kiungo cha https://atmis.kilimo.go.tz . Kwa wale watakaokuwa wanahuisha leseni zao watajaza fomu maalum ya kuomba kuhuisha leseni zao itakayopatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Kahawa www.coffeeboard.or.tz .

  5. Vyama vya ushirika vinatakiwa kuanza kukusanya kahawa kutoka kwa wakulima mara tu inapokuwa tayari. Aidha, vyama vya ushirika vitapaswa kuhakikisha kuwa akaunti zao za malipo zipo hai ili kuwezesha zoezi la uuzaji wa kahawa na malipo kufanyika mapema na kuepuka ucheleweshwaji wa malipo ya fedha za wakulima.

  6. Vyama vya msingi vilivyopewa kibali cha kuuza kahawa mnadani msimu uliopita vitahuisha vibali vyao kwa kujaza fomu maalum. Fomu hizi zitapatikana kwenye ofisi za Kanda za Bodi ya Kahawa na kwenye viwanda vya kukobolea kahawa.

  7. Vyama vya ushirika vikamilishe mapema taratibu za upatikanaji wa mitaji ili vianze ukusanyaji wa kahawa ya wakulima wao mara tu kahawa inapokuwa tayari.

  8. Bodi ya Kahawa itaanza mara moja kuendesha minada ya kahawa pindi kiasi cha kutosha cha kahawa kitakapokuwa tayari.

  9. Vyama vya ushirika vihakikishe kuwa mitambo ya kuchakata kahawa (CPU) iliyoko chini yao inatumika na inafunguliwa mara tu kahawa inapokuwa tayari ili kufanikisha lengo la Serikali la kuongeza ubora wa kahawa na bei ya mkulima.

 

 

Kaimu Mkurugenzi Mkuu
Bodi ya Kahawa Tanzania
S. L. P. 732 – Moshi
Simu: 027-27-52324
Nukushi: 027-27-52026
Barua pepe: info@coffeeboard.or.tz
Tovuti: www.coffeeboard.or.tz